Msichana mmoja mkazi wa eneo la Minga katika Manispaa ya Singida (muuza duka), amenusurika kifo baada ya kumwagiwa uji wa moto na mke wa tajiri yake na kumsababishia maumivu makali kutokana na kile kinachosadikiwa kuwa ni wivu wa kimapenzi.
Muuguzi wa zamu katika Hospitali ya mkoa wa Singida, wodi namba mbili ya wanawake, Anna Sprian amefahamisha kuwa binti huyo amejeruhiwa sehemu za sikio la upande wa kulia na mgongoni, ambapo amesema hali ya mgonjwa huyo inaendelea vizuri kutokana na matibabu anayoyapata hospitalini hapo.
Amesema akiwa anaendelea na kazi zake za kuuza bidhaa mbalimbali dukani hapo, ghafla alitokea mke wa bosi wake akiwa na chupa yenye uji wa moto na kuwa alimmwagia usoni ambapo baada ya kumwagiwa uji huo alitaka kujiokoa ili usimmwagikie usoni na ndipo ulimuunguza kwenye sikio la kulia na mgongoni na kuwa baada ya mke wa bosi wake kumkosa uso alitoa kisu kutaka kumchoma kifuani.
“Mimi sikuwa na ugomvi naye wala sijui chanzo cha yeye kufika dukani na kunifanyia vile jana, maana kama ni kazi mimi ninafanya kulingana na maelekezo kutoka kwa bosi wangu Chale lakini sijui kilichomfanya afikirie kunifanyia huu unyama” alisema.
Aidha, amesema katika purukushani za kujiokoa asichomwe kisu hicho, alifanikiwa kumkamata mkono mwanamke huyo na kupiga kelele za kuomba msaada ambapo watu walifika na kumwokoa baada ya muda mchache ambapo alichukuliwa na bosi wake hadi Kituo cha Polisi mjini Singida na kupewa PF3 kwa ajili ya matibabu na kupelekwa katika hospitali hiyo ambako amelazwa huku akiwa ma majeraha mwilini.
Wakiongea kwa nyakati tofauti baadhi ya majirani wa familia hiyo, wameonyesha masikitiko yao juu ya tukio hilo na hatua ya mwananmke huyo kummwagia uji msichana huyo huku wakihusisha tukio hilo na wivu wa kimapenzi baina ya mfanyakazi huyo na mume wa mtuhumiwa.
“Kama aliona kama kuna sehemu kamkosea angemuonya au kama ameshindwa kueleweka basi angemshitaki hata polisi kwani kitu alichokifanya hakiendani na haki za binadamu kwakuwa ni kumdhalilisha huyu msichana ambaye alikuwa akifanya kazi kwa ajili ya kujipatia kipato chake na familia yake." alisema shuhuda mmoja
Kamanda wa Polisi Mkoani hapa, Geofrey Kamwela, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuwa wanamshikilia mtuhumiwa kwa mahojiano na mara baada ya upelelezi kukamilika atafikishwa Mahakamani kujibu tuhuma hizo.
Post a Comment