KUJIFUNZA ndiyo mwanzo wa maarifa. Siku zote nimekuwa nikisisitiza hivyo. Ndugu zangu, marafiki ambao wameungana nami katika ukurasa huu na safu nyingine ninazoandika katika Magazeti ya Global Publishers kuhusiana na uhusiano wamevuna mengi.
Fikra zao hazipo vilevile tena. Wana mabadiliko makubwa kwa sababu wamezoa maarifa ambayo yanawasaidia kufanya uamuzi sahihi kwenye uhusiano na wapenzi wao.
Kama ndiyo mara ya kwanza kuanza kusoma ukurasa huu, tafadhali usikose kila wiki, pia unaweza kujiunga nami kwenye Love & Life kwenye Gazeti la Uwazi kila Jumanne, All About Love katika Gazeti la Risasi kila Jumatano na Elimu ya Mapenzi kwenye Gazeti la Championi, toleo la Jumamosi.
Sasa turejee kwenye mada yetu, ingawa ni mambo ambayo nimeshazungumza mara nyingi huko nyuma, leo nakuletea sifa muhimu zaidi ambazo ni vizuri kuziangalia kwa mwenzi wako ili kujua kama ana upendo wa kweli.
Ukweli ni kwamba vijana wengi ambao wanapendana leo, mapenzi yao hayadumu kiasi cha kubatizwa jina la utamu wa banzoka. Lakini yote hii inatokana na ukweli kwamba elimu ya mapenzi ambayo ni muhimu kwa binadamu haitolewi ipasavyo.
Ipo dhana potofu kwamba kumfundisha mtoto mapenzi ni kumharibu, jambo ambalo si kweli bali inategemea mtoto huyo anafundishwa nini na kwa wakati gani.
Lakini cha kushangaza zaidi hata watu wazima ambao ni wadau wa mapenzi hawayajui matokeo yake wanajiingiza kwenye uhusiano wakiwa bumbumbu na hivyo kuteswa na changamoto zinazowakabili ndani yake.
Leo tutajifunza kwa undani sifa kumi za mpenzi bora ili tuweze kuwatambua wapenzi wetu kabla ya kuwapa mioyo na utu wetu. Twende tukaone.
1. Mpenzi wa kweli ni yule ambaye hatangoja kujua nini unahitaji yaani hana sababu ya kusubiri kuombwa ndiyo atoe msaada.
Kwa kuwa ana mapenzi ya dhati na anajua mahitaji yako, hawezi kusubiri kushurutishwa au ionekane kama vile anatoa hongo. Kipengele hiki kinawahusu wanaume zaidi.
2. Ni yule atakayejua wakati gani huna furaha au una furaha na atakuwa na wewe kwa hali zote mbili. Hata kama ukiwa huna furaha, hujiona mwenye jukumu kuhakikisha unakuwa nayo kwa namna yoyote ile.
3. Ni yule atayekuwa tayari kukusikiliza kwa kile utakachosema, hatajali umezungumza baya au zuri. Kwa bahati nzuri ni kwamba, ikiwa umekosea, yeye atachukua jukumu la kukuweka sawa.
Asiye na penzi la dhati, ukikosea kwake ni kichekesho. Badala ya kukurekebisha na kukuweka kwenye mstari, atakucheka.
4. Atakuwa na wewe wakati wa shida na raha. Hatakuwa mtu wa kuviziavizia na kujisogeza wakati ukiwa na raha.Kwake, shida yako itakuwa yake akiwa na imani kuwa, hata yake ni yako pia. Anayejiweka kando ukiwa na matatizo, siyo sahihi, mwepuke.
5. Mpenzi wa kweli atakuheshimu na hatapenda kuwa kikwazo cha maisha yako, atakulinda daima. Heshima ni msingi mkuu.
6. Atakupenda kwa moyo wake wote na wala si kwa ajili ya shinikizo fulani. Pesa si kipaumbele chake.
7. Mpenzi wa kweli ni yule atakayeonyesha kuthamini nafasi yako kama rafiki au mpenzi mbele ya wengine, hafichi hisia zake mbele za watu, atakutetea na kukufanya wa kwanza.
8. Kwenye ukweli mpenzi mzuri atasema bila kukuficha na atapenda kukuonyesha mifano ya namna ya kuwa mkweli na mwaminifu.
9. Mpenzi wa kweli ni yule anayejiamini, asiyeyumba katika maamuzi hata kama atalazimika kufanya maamuzi magumu.Kikubwa ni kusimamia katika ukweli na masilahi yanayoeleweka.
10. Atakuwa tayari kuvumilia, hatakuwa mwepesi wa hasira wala kutumia lugha chafu na ubabe. Ni mwelekezaji zaidi, hawezi kukurushia maneno ya kuudhi maana anajua kukuudhi au kukuumiza ni kuharibu maana nzima ya penzi lenu.Bila shaka vipengele hivyo vimekubadilisha sana. Hadi wiki ijayo kwa mada nyingine, USIKOSE!
Post a Comment